Mhe. Prof. Adolf Mkenda, Waziri wa Kilimo alifanya ziara ya kikazi nchini Bujumbura, Burundi kuanzia tarehe 18 - 21 Oktoba, 2021.  Lengo ya ziara hiyo ni kukutana na kufanya mazungumzo ya kubalishana  uzoefu na Waziri wa Kilimo wa Burundi, Mhe. Dkt Rurema Deo-Guide kuhusu utekelezaji wa mifumo ya utoaji ruzuku kwenye pembejeo za Kilimo.  Waziri Mkenda anatarajiwa kutembelea kiwanda cha Mbolea cha FOMI ambacho kupitia kampuni yake ya ITRACOM imeanza ujenzi wa kiwanda cha mbolea Jijini Dodoma nchini Tanzania na kujadiliana namna ya kuhakikisha ujenzi na uzalishaji wa kiwanda hicho.  Pia atakutana na Taasisi za utafiti wa nchini Burundi zinazoshirikiana na kiwanda cha FOMI katika kufanya tafiti za afya ya udongo na kuibua maeneo ya ushirikiano katika kilimo kwa lengo la kukuza uchumi baina ya nchi zote mbili.

 Katika ziara hiyo Waziri wa Kilimo ameambatana na Mkurugenzi wa Mazao wa Wizara ya Kilimo Bw. Enock Nyasebwa, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mbolea Tanzania Dkt. Stephan Ngailo pamoja na mtaalamu wa udongo Dkt. Catherine Senkoro ambaye ni Mkurugenzi wa kituo cha Utafiti wa Kilimo - TARI Mlingano kilichopo mkoani Tanga.

  • Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda akisisitiza jambo mbele ya Waziri wa Kilimo wa Burundi Mhe. Dkt Rureme Deo – Guide mara baada ya kukutana na kufanya mazungumzo katika ofisi ya wizara hiyo iliyopo mtaa wa Commune Mukaza kata ya Rohero mjini Bujumbura akiwa katika ziara ya kikazi ya siku mbili.
  • Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda akiwa ameambatana na Waziri wa Kilimo wa Burundi Mhe. Dkt Rureme Deo – Guide wakikagua baadhi ya mazao ambayo yamefanyiwa utafiti na Taasisi ya Kilimo nchini Burundi ya ISABU tarehe 20 Oktoba, 2021.
  • Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda akiwa ameambatana na Waziri wa Kilimo wa Burundi Mhe. Dkt Rureme Deo – Guide wakikagua viazi lishe vinavyozalishwa na taasisi yaUtafiti wa Kilimo ya Nchini Burundi ya ISABU kwa ajili ya utafiti tarehe 20 Oktoba, 2021.