Tarehe 15 Juni, 2024 Mhe. Balozi Gelasius G. Byakanwa, Balozi wa Tanzania nchini Burundi alifungua mashindano ya Insha  kwa Wanafunzi wa Vyuo Vikuu vilivyopo Bujumbura.  Hatua hii inakuja ikiwa ni maandalizi ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar yatakayofanyika 25 Juni, 2024, Bujumbura.  
Katika Maadhimisho hayo Ubalozi uliandaa shindano la kuandika Insha ya Kiswahili kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya hapa Burundi, ikiwa ni hatua ya kutambua kuwa Warundi wengi  wanafahamu na wanaongea Kiswahili fasaha. Vilevile mashindano hayo ni mpango wa ubalozi wa kukuza na kutangaza lugha ya Kiswahili  nchini Burundi. Katika Mashindano hayo, Wanafunzi 121 walishindanishwa kwa kuchagua mada tatu zilizochaguliwa na jopo la wataalam wa ubalozi ambazo ni: Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere:na Umoja na Amani ndiyo nguzo ya maendeleo. Siku ya tarehe 25 Juni, 2024 wakati wa maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar utachezeshwa mchezo wa bahati nasibu wa kuwapata washindi wawili miongoni mwa washindi watano. Washindi hao wawili ndio watakaobahatika kutembelea Zanzibar kwa siku mbili.

  • WANAFUNZI WA VYUO VIKUU BUJUMBURA WALIOSHIRIKI KWENYE MASHINDANO YA UANDISHI WA INSHA WAKIWA KWENYE MASHINDANO HAYO YA UANDISHI.